WAZIRI SILAA AZINDUA RASMI BODI MPYA YA TTCL
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amezindua rasmi Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania - TTCL leo tarehe 16 Desemba, 2024, Makao Makuu ya TTCL, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Silaa amempongeza Bw. David Nchimbi kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasilano Tanzania - TTCL pamoja na Wajumbe walioteuliwa kuunda Bodi hiyo ya Wakurugenzi.
Aidha, Mhe. Silaa ameitaka Bodi mpya ya TTCL kutumia ujuzi,weledi na kuandaa mpango mkakati ili kuhakikisha adhma ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kulifanya Shirika la Mawasiliano Tanzania - TTCL kuwa shirika la kibiashara inafikiwa.
“Kutokana na maelekezo aliyoyatoa Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kunielekeza Waziri kusimamia Shirika hili na kuhakikisha linajisimamia kibiashara, natoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa Bodi na Bodi kwa ujumla kukaa kwa haraka na kutengeneza mpango ambao utatutoa hapa tulipo na kutupeleka kwenye eneo la uendeshaji wa Shirika hili kibiashara na kutekeleza maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais” Amesema Mhe. Silaa.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL, Bw. David Nchimbi, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na imani kubwa iliyoweka kwa Wajumbe wanaounda Bodi hiyo.
Bw. Nchimbi ameahidi kuwa Bodi yake itahakikisha Shirika linaendelea kwenda mbele zaidi na kukata kiu ya Watanzania ya kuona Shirika linajiendesha kibiashara.