WAZIRI MKUU ATEMBELEA BANDA LA TTCL SABASABA 2023
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) ametembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL lililopo ndani ya TEHAMA PAVILION katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Ametembelea banda hilo Jumatano, Julai 05, 2023 alipomwakilisha Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 47, Temeke Dar es Salaam. Akiwa bandani hapo Waziri Mkuu alipokea maelezo ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya usambazaji wa huduma ya Mkongo wa Taifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Peter R. Ulanga. Mhandisi Ulanga alisema kuwa kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 TTCL wanampango wa kufikisha Mkongo wa Taifa katika Wilaya 99 hadi kufikia Disemba 2023. Aidha alisema kuwa TTCL kama Shirika Mama la Mawasiliano litahakikisha linasimamia kikamilifu uhifadhi wa Data kimtandao kupitia kituo cha Kuhifadhi data kimtandao cha NIDC kinachosimamiwa na Shirika hilo ili kufanikisha mapinduzi hasa katika uchumi wa Kidijitali.