N-CARD YAPONGEZWA UKUSANYAJI NA UDHIBITI WA MAPATO
Imeelezwa kuwa uwepo wa matumizi ya N-CARD katika maeneo ya vivuko, stendi za mabasi na Viwanja vya mpira wa miguu umesaidia katika ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya serikali.
Hayo yalibainishwa na Mhe. Abrahman Hussein Kololi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati wakati wa ziara ya Uongozi wa halmashauri hiyo ya Babat ilipotembelea vituo vinavyotoa huduma za ukusanyaji wa Mapato kwa njia ya N-CARD hivi karibuni.
"Tumeshuhudia namna ambayo mifumo ya N-CARD imekuwa ikifanya kazi katika ukusanyaji na udhibiti wa mapato, hakika tunaupongeza Uongozi na Wafanyakazi wa N-CARD chini ya usimamizi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL kwa kazi kubwa mnayoifanya kwani sisi ni mashuhuda namba ambavyo mfumo huu umekuwa ukisaidia katika uthibiti wa upotevu wa mapato” amesema Mhe.Kololi
Ziara hiyo imewapa fursa ya kutembelea vituo mbalimbali vinavyotumia mfumo wa N-CARD kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na Magogoni Ferry na Uwanja wa Benjamin Mkapa, na kujionea jinsi mifumo huo unavyofanya kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, CPA. Shaaban Mpendu, alieleza kuwa halmashauri yao ina mpango wa kutumia mfumo huo wa N-CARD ili kuongeza ufanisi zaidi katika ukusanyaji wa mapato.
Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Stendi hivyo kupitia ziara hii wamejifunza kuhusu ubora na uzuri wa mifumo hii katika ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya serikali.
Alisema wapo kwenye maandalizi ya kuanzisha matumizi ya mifumo hii katika maeneo mengine ya halmashauri ikiwa ni pamoja na uwanja wa Tanzanite kwa Raha ambao umekuwa ukitumika katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Vedastus Mwita, ambaye ni Mkurugenzi wa Biashara, aliuelezea Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Babati jinsi N-CARD inavyotoa huduma za ukusanyaji na udhibiti wa mapato katika maeneo mbalimbali.
Naye Bi. Happy Nzunda, Meneja Mkuu wa T-PESA, Kampuni Tanzu ya TTCL amesema matumizi ya mifumo ya N-CARD yamekuwa na tija kubwa, kwani imeweza kudhibiti ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi mkubwa.
Alisema kuwa ushirikiano wa Halmashauri ya Mji wa Bababti na N-CARD utakuwa na manufaa makubwa katika biashara na utasaidia kuboresha zaidi huduma za ukusanyaji mapato.